Kasekese. Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Bw. Salehe Mhando amewaagiza wananchi wote waliopo vijiji vyote vya Halmashauri ya wilaya ya Mpanda kujiunga na mfuko wa bima ya Afya ya Jamii (CHF). Mhando ameyasema hayo Julai 29, 2017 wakati wa uzinduzi wa Hamasa ya wananchi kujiunga na bima ya Afya ya Jamii.
Kabla ya kuzindua uhamasishaji, Mhando alizungukia kwanza zahanati ya Kasekese kujionia kama zahanati ina dawa za kutosha na alikuta dawa zipo za kutosha.
“Kabla ya kuanza kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya Afya ya jamii, nimejilizisha kwanza kutembelea zahanati na kuangalia kama zina dawa za kutosha. Nimefika na kukagua zahanati na vituo vya afya vina dawa za kutosha”. Alisema Mhando.
Kila kaya ikichangia shilingi 10,000 kwa ajili ya mfuko wa bima ya afya ya jamii ina uwezo wa kutibisha watu watano kwa mwaka mzima. Katika hali ya kawaida ukichukua elfu 10 ukagawanya kwa watu 5 katika familia utakuta kila mwanachama wa bima anatibiwa kwa gharama ya shilingi 2000 tu.
Katika hao wanachama, mchangiaji anaruhusiwa kuwa na wategemzei wane (4) walio na umri chini ya miaka 18 na wanafunzi wote wa shule za msingi na sekondari wanawawekwa katika kundi la wategemezi. Kwa wale wasio wanafunzi na kama wana umri wa miaka 18 na kuendelea wanapaswa kujiunga na bima ya afya ya Jamii (CHF).
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda Dk.Seleman Mtenjela alishauri wananchi wajiunge kwa wingi kuchangia mfuko wa bima ya afya jamii. Wananchi wakichangia kwa wingi ndivyo na zahanati inavyopata fedha nyingi za kununulia dawa za zahanati au kituo cha afya. Kwa sasa utaratibu umebadilika, kamati za afya zilizopo vijijini ndizo zenye mamlaka ya kuamua matumizi ya ununuzi kwa ajili ya zahanati au kituo.
“Wanachama wakichangia shilingi 5,000,000 na serikali nayo inawachangia 5,000,000. Hii inaitwa tele kwa tele”. Alisema Mtenjela
Hata hivyo, ni vema wananchi wakaelewa kuwa kuna baadhi ya dawa zinazoruhusiwa kuwa kwenye zahanati, zingine kwenye vituo vya afya na dawa zingine zinapatikana kwenye hospitali kubwa tu. Jambo hili linatokana na uwezo wa watalaam wa afya. Wagonjwa wanapoenda kupata matibabu kwenye zahanati, watalaam wakiwashauri kuwa ugonjwa wao hauna dawa katika zahanati na hivyo hupaswa kuwaelekeza kwenda kituo cha afya au hospitali kwa ajili ya matibabu zaidi.
Serikali ilitangaza watoto watibiwe bure lakini kama wazazi hamtajiunga kwa wingi ili zahanati ipate pesa za kununulia dawa, watatibiwa bure kwa dawa za kutoka wapi? Zahanati ikiwa na dawa za kutosha wale wote wanaostahili kupata matibabu bila malipo wataendelea kuhudumiwa.
Hata hivyo Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Bw.Mhando aliwaonya viongozi wa vijiji kuwa makini wakati wa kuhakiki wazee wanaotakiwa kupata matibabu bure.
“Wakati mheshimiwa Rais John Magufuli anashughulika na zoezi la watumishi hewa, kuna wazee hewa katika huduma za matibabu”. Alisema Mhando
Wazee wanaanzia umri wa mika sitini lakini kuna wazee wa miaka 80 ambao ni matajiri. Yaani wana mifugo au uwezo wa kimaisha, sasa watu wa namna hiyo au wenye sifa zinazofanana hatuwezi kuwaruhusu kutibiwa bure.
Wananchi wote wanatakiwa kuwekeza katika bima ya afya ya jamii kwani ugonjwa unajitokeza wakati huna fedha. Mkombozi wa afya wakati wote kwa mwaka mzima ni mfuko wa bima ya afya ya jamii. Ni muda mwafaka wa kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika afya yako na wategemezi 4. Na kama kuna maoni au maswali kuhusiana na mfuko wa bima ya afya ya jamii, fika zahanati au kituo cha afya kilichopo ndani ya wilaya ya Tanganyika kwa ufafanuzi zaidi.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.