Mkurugenzi wa kiwanda cha pamba (NGS) wilayani Tanganyika, Mhe. Njalu Silanga amepongezwa kwa kufanya uwekezaji wa kuwanufaisha kiuchumi wakulima wa pamba na wajasiriamali. Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo wakati alipotembelea na kujionea kiwanda hicho Machi 02, 2021.
Uwepo wa kiwanda hiki kikubwa wilayani Tanganyika kimekuwa mkombozi kwa wakulima wa pamba kwani kabla ya kuwepo kwa kiwanda hiki, wakulima walitegemea wanunuzi wa kutoka mikoa ya kanda ya ziwa ambapo pamba nyingi ya wakulima ilikuwa inaharibika kwa kunyeshewa na mvua. Kwa sasa pamba yote inayolimwa katika mikoa ya Katavi na Kigoma inanunuliwa na mmiliki huyo wa kiwanda cha pamba kilichopo wilayani Tanganyika.
Aidha, Prof. Mkumbo ameendelea kumpongeza mwekezaji huyo kwa kuzalisha ajira ya watu 180 na kufanya mzunguko wa kiuchumi kwa wananchi wa wilaya ya Tanganyika.
“ Kuwepo kwa kiwanda hiki kikubwa chenye wafanyakazi 180 wa kiwanda kunasababisa wajasiriamali wanaouza chakula kupata fedha kwani wafanya kazi wa kiwandani wanahitaji kunywa chai na chakula cha mchana kwa kununua. Waendesha bodaboda na bajaj nao wanapata fedha kwa kuwasafirisha wafanyakazi na watu wengine wanaokuja kupata huduma mbalimbali”. Prof. Mkumbo
Mhe. Silanga amenza kuweka mikakati ya kuhakikisha kila mwananchi aliyopo Tanganyika ananufaika na uwepo wa kiwanda hicho kikubwa cha pamba moja kwa moja au kwa namna nyingine. Kwa msimu huu amewawezesha maafisa ugani na wakulima bora wa zao la pamba wa kata zote 16 za halmashauri ya wilaya ya Tanganyika kwa kuwapa mafuta ya pikipiki na posho ili waweze kuwatembelea mara kwa mara wakulima wa zao la pamba na kutatua changamoto wanazokutana nazo.
“Kwa msimu ujao nitalima hekta 500 za zao la pamba wilayani Tanganyika kwa lengo la kuwa shamba darasa ili wakulima wajifunze kwangu. Nitakuwa nalima mwezi wa tano na kuvuna mwezi wa tisa kwa kilimo cha umwagiliaji. Ikifika mwezi wa kumi na moja nalima tena ndani ya shamba hilo hilo. Lengo niweze kuwaonesha wakulima wa pamba kuwa unaweza kutumia shambo moja kwa kulima pamba kwa misimu miwili kwa mwaka”. Mhe. Silanga
Hata hivyo, Mhe. Silanga ameanza kujipanga kutoa huduma za msaada kwa jamii (Community Social Responsibility-CSR) walau kwa kuanza na utowaji wa madawati. Madawati hayo yatapelekwa kwa baadhi ya shule za kata za Mpandandogo, Sibwesa na Kasekese. Lakini pia atasikiliza ushauri wa viongozi na uhitaji wa msaada huo uelekezwe wapi. Lengo la msaada huu ni kuendeleza kudumisha ushirikiano kwa jamii na viongozi.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.