Kabungu. Mkuu wa mkoa wa Katavi Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda Bw. Romuli Rojas John kwa kuanzisha mnada mkubwa wa sabasaba. Pongezi hizo zimetolewa Julai 7, 2017 wakati wa uzinduzi wa mnada huo wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda.
“Mkurugenzi, umebuni kitu kizuri sana kwa Mkoa wa Katavi. Watu walikuwa hawana sehemu ya kwenda kula nyama choma na kupumzika na watoto wao siku za Jumamosi. Pia eneo hili litakuwa linatumika wakati wa maonesho ya saba saba ya Mkoa wa Katavi”. Alisema Meja Jenerali Mstaafu Muhuga.
Mkoa wa Katavi ulikuwa hauna viwanja vya maonesho ya wafanya biashara ya kila mwaka (Saba saba) sasa ni matumaini kuwa maonesho yatakuwa yanafanyikia katika viwanja hivi kila mwaka. Mnada huu utakuwa unafanyika kila Jumamosi ya wiki na siku zinaweza kuongezwa kutegemeana na uhitaji wa wafanya biashara.
Eneo la mnada lina ukubwa wa Hekari 14 na maeneo yametengwa kutegemeana na aina ya biashara. Kuna eneo lililotengwa kwa ajili ya mifugo, nyama choma, vinywaji na michezo ya watoto. Maeneo mengine ni kwa ajili ya biashara za mitumba, vyombo vya ndani, migahawa na mazao ya chakula. Kuna maeneo ya maegesho ya magari makubwa na madogo, sehemu ya kupumzikia na huduma mbali mbali.
Mnada huu utaiweka wilaya ya Tanganyika katika ramani ya Dunia kwani watalii watakao fika Mkoani Katavi watalazimika kufika kupata huduma mbali mbali katika viwanja hivyo vya Saba saba. Wananchi nao wataongeza kipato kutokana na kuuza bidhaa mbali mbali na mzunguko wa fedha utaongezeka sana.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda Bw.John amesema ataendelea kuutangaza ndani na nje ya Tanzania. Lengo ni kuhakikisha kila mfanya biashara katika mnada wa saba saba apate wateja wa kutosha.
“Nitahakikisha matamasha makubwa, ngoma za asili na michezo mbali mbali inafanyikia katika viwanja hivi vya saba saba”. Alisema Bw.John
Mnada uliozinduliwa unapatikana katika kijiji cha Kabungu, kitongozi cha Shongo tupendane mbele kidogo ya kiwanda cha kokoto mkono wa kushoto kama umetokea Mpanda mjini kuelekea Kigoma. Mnada wa saba saba unafikika kiurahisi kwani kuna barabara ya lami na umeme wa uhakika.Kwa wale mliowahi kufika mnada wa Dodoma au Arusha kwa Mrombo, mtagundua kuwa mnada wa saba saba ulipo Tanganyika ni zaidi ya minada yote ya Tanzania.
Ni mnada wa mazingira ya asili, misitu ya asili na unapata nyama choma iliyoandaliwa na watalaam waliobobea katika tasnia hiyo.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.